MATUMAINI KATIKA KIPINDI CHA KIPINDUPINDU

(Hope in the time of the Cholera)

Na Temba A Nolutshungu

Takriban nchi zote ulimwenguni zimepata maendeleo ya kiuchumi katika mwongo mmoja uliopita, licha ya kudhoofika kwa uchumi duniani.  Hata hivyo, Wazimbabwe wameshuhudia mapato yao  yakishuka kwa zaidi ya thuluthi mbili katika matokeo mabaya zaidi ya kiuchumi ya mataifa yote yenye taarifa kama za nchi hiyo.  Lakini wanaweza kuokoa taifa lao wakipewa nafasi.

Taarifa ya kutia moyo ni kwamba marekebisho ya kiuchumi huleta matokeo ya haraka; jirani zake wameona athari za kufungua biashara katika miaka kumi iliyopita na Zimbabwe yenyewe iliuza bidhaa nyingi miaka michache iliyopita.  Kila urahisishaji wa kodi na kanuni za biashara, kila uimarishaji wa sheria za mikataba na usalama wa wanajamii una athari ya mara moja kwa watu binafsi, familia na uchumi.


Mkurupuko wa kipindupindu wa muda mrefu nchini Zimbabwe ni mfano mmojawapo wa athari za ukandamizaji uliojikita.  Tangu 1998 muda wa wastani wa maisha ya Wazimbabwe umeshuka kutoka miaka 55 hadi 35.  Zaidi ya asilimia themanini ya watu wazima hawana ajira.  Takriban nusu ya Wazimbabwe wako kwenye hatari ya utapiamlo na njaa kali: watu milioni nane – ambao ni maradufu ya waliokuwepo miaka michache iliyopita – wanahitaji msaada wa chakula.  Watoto wa Zimbabwe wanakufa kwa wingi zaidi, wanautapia mlo na ukuaji wao umedumazwa sana wakilinganishwa na watoto

wengine barani Afrika.

Utawala wa kifisadi wa Robert Mugabe umeshikilia madaraka kwa kutumia sheria ya kijeshi, wizi wa ardhi, kudhibiti vyombo vya habari na kuzuia  upinzani.  Wakereketwa wa upinzani wametiwa korokoroni na kuuawa na mahakama yenye ujasiri imepuuzwa.  Serikali ya mseto iliyopo inaonekana kama ujanja wa Rais Robert Mugabe kumaliza maadui zake kwa kuwavuta karibu naye.  

Kikundi cha Kupigania Haki za Binadamu kisicho cha serikali nchini Zimbabwe (Zimbabwe Human Rights NGO Forum) kimeorodhesha zaidi ya mifano 20,000 ya ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na visa 3,000 vya utesaji tangu 2001.  Badala ya kulinda wananchi dhidi ya matumizi ya nguvu, vyombo vya usalama vya Zimbabwe hasa vinalinda tabaka  tawala na kuwadhulumu wananchi.

Si ajabu kwamba maelfu hutorokea Botswana na Afrika Kusini huku maelfu zaidi wakirejeshwa makwao:   takriban thuluthi moja huishi katika mataifa ya ng’ambo.

Viongozi wa Zimbabwe hudai kwamba tatizo hili linatokana na ukoloni wa Uingereza wala sio dhuluma ya Mugabe, matumizi mabaya ya fedha za umma, kodi, vizuizi vya biashara na mfumko wa uchumi.  Amebadilisha nchi iliyokuwa ikikuza chakula kingi kuwa nchi isiyoleta matumaini kwa mamilioni.

Lakini Zimbabwe si nchi isiyokuwa na matumaini: ina wajasiriamali, wanamigodi, wakulima, walimu na hata watumishi wa umma wachache.  Majirani zake ni marafiki (japo wakati mwingine ni marafiki wakubwa mno wa Mugabe) na Zimbabwe imepiga hatua kubwa kwa kuruhusu fedha za kigeni kutumika badala ya fedha zake zenye mfumko mkubwa.

Sasa nchi hii inahitaji kudhibiti matumizi ya serikali na kuimarisha uhuru wa kiuchumi ili kumwokoa kila mfanyakazi kutokana na kanuni na kodi zinazodhulumu na kusambaratisha shughuli za kiuchumi.  Shirika la Kimataifa la Fedha (International Finance Corporation) linakisia kwamba inachukua siku 96 kuanzisha biashara nchini Zimbabwe, siku 481 kununua leseni zote zinazohitajika na siku 30 kusajili mali.  Ikiwa uanzishaji wa biashara mpya ni mgumu, inakuwa vigumu zaidi kutoa ajira.  Hata ikiwa gharama ya kuajiri mfanyakazi ni sawa na mara 14 ya wastani wa mshahara nchini.  Mahitaji ya kuanzisha biashara kwa kampuni mpya yamewakatisha tamaa Wazimbabwe na kuwaondoa kwenye mfumo rasmi wa uchumi.

Mataifa yanayoendelea yaliyopunguza maksudi vizuizi vya biashara mnamo miaka ya 1990 yalipata maendelo mara tatu zaidi (kwa asilimia tano kila mwaka ) kuliko yale ambayo sera zake za biashara hazikubadilishwa.  Zimbabwe ilizuia biashara ya kimataifa.  Hivi sasa ni nchi ya saba mbaya zaidi katika Orodha ya Benki ya Dunia ya Vizuizi vya Biashara (World Bank’s Trade Restrictiveness Index). Upunguzaji wa siku thelathini zinazohitajika kutayarisha taarifa za uuzaji wa bidhaa katika mataifa ya nje au siku 42 zinazohitajika kuagiza bidhaa kutoka nje utawapa wajasiriamali fursa ya kushindana.

Unyakuaji wa mashamba ya Wazungu na wanasiasa ndio unaopata nafasi kubwa katika vichwa vya habari lakini hali ya kusikitisha ni kwamba haki za mali kwa kila mtu, iwe ni vipande vya ardhi au biashara zimetupiliwa mbali.  Wazimbabwe wengi hawawezi kupata hati za kumiliki ardhi, hata wale waliopewa ardhi ilioibwa kutoka kwa wengine.  Kwa sababu hawawezi kutumia au kuuza haki za mali, watu maskini hawawezi kupata mikopo ili waweze kuboresha ardhi zao na uzalishaji.

Funzo linalofahamika la kuboresha biashara, uanzishaji biashara, ajira na usajili wa ardhi ni rahisi;  rahisisha, rahisisha, rahisisha.

Lakini kurahisha si kitu chepesi hivyo.  Watu wachache wenye uwezo mkubwa na vitisho vingi wananufaishwa na mfumo uliosababisha hali hii mbaya – lakini wakati fulani katika siku za usoni utawala wa chama cha ZANU – PF cha Robert Mugabe utadhoofika na kuporomoka na kufungua njia ya mabadiliko.  Wanamabadiliko sharti wawe tayari na sera nzuri zilizofaulu katika mataifa mengine na zinazoweza kutumika nchini Zimbabwe.

Kinyume na Korea ya Kaskazini au Myanmar, Zimbabwe ina mafundi wengi, wakulima, wafanyabiashara, mahakimu, watumishi wa umma na hata askari wanaokumbuka namna nchi ilivyofaulu inavyofanya kazi na namna inavyoweza kuchukua nafasi yake kamili.  Ndiyo twaweza.

 http://www.africanliberty.org/pdf/zimbabwepapers.pdf  Ni Tume ya “Karatasi za  Zimbabwe – Ajenda Chanya ya Kufufua Zimbabwe”,  iliyochapishwa na Vikundi Tisa Mashuhuri vya Kutafakari Barani Afrika, mnamo Mei 19.

RELATED ARTICLES